Matangazo ya biashara yaondokane na fikra potofu za kijinsia - UNWomen

21 Juni 2017

Wiki ya tamasha la kazi za ubunifu likiendelea leo huko Cannes nchini Ufaransa, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UNWomen, Phumzile Mlambo-Ngcuka ametaka sekta ya matangazo ya biashara iondokane na fikra potofu za kijinsia.

Amesema hayo katika taarifa iliyotolewa na UN-Women akiongeza kuwa sekta ya matangazo ya biashara inatumia teknolojia za kisasa kufikisha ujumbe ikiwemo ule wa kuwezesha watumiaji kuchagua huduma na bidhaa.

Bi. Ngucka amesema mara nyingi matangazo hayo hutumika kuonyesha mtazamo hasi dhidi ya wanawake na wakati mwingine wanaume jambo ambalo amesema halifai.

Amesema fikra hizo zinaongeza pengo la usawa wa kijinsia na hivyo ni vyema viongozi katika sekta hiyo ya matangazo kuchambua jinsi ya kuweka vigezo na hatimaye kuleta mabadiliko chanya katika fikra za kitamaduni.

Tamasha hilo la ubunifu limeanza tarehe 17 mwezi huu na linamalizika Jumamosi hii.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter