Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jayathma Wickramanayake ndiye mwakilishi mpya wa vijana UM

Jayathma Wickramanayake ndiye mwakilishi mpya wa vijana UM

Jayathma Wickramanayake kutoka Sri Lanka ndiye mteule mpya wa kubeba bendera ya vijana kwenye Umoja wa Mataifa baada ya kutangazwa Jumanne na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.

Jayathma anakuwa mrithi wa Ahmad Alhendawi kutoka Jordan ambaye Katibu Mkuu amemshukuru kwa kazi nzuri ya kushughulikia mahitaji na haki za vijana na kuzifikisha kazi za Umoja wa Mataifa kwa vijana hao alipohudumu kama mwakilishi maalumu wa vijana wa Umoja wa Mataifa.

Guterres amesema mafanikio ya ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu yanategemea kuwezeshwa kwa vijana, kama watenda haki, mawakala wa mabadiliko na wabeba tochi. Tangu akiwa na umri wa miaka 21 Bi. Wickramanayake amekuwa akijihusisha na kuchagiza vijana kimataifa ikiwemo wakati wa kupitishwa azimio la Umoja wa Mataifa la siku ya ujuzi kwa vijana duniani. Pia amekuwa na mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko ya maendeleo ya vijana kitaifa nchini Sri Lanka kwa kuanzisha kampeni iitwayo“HashtagGeneration.”

Hivi sasa anafanya kazi kama afisa kwenye huduma ya uongozi ya Sri Lanka, na kabla ya hapo aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali zinazohusu masuala ya vijana ikiwa ni pamoja na kuwa katibu muhtasi wa katibu mkuu wa bunge la nchi hiyo, na kuwa seneta kwenye bunge la vijana la Sri lanka kati ya mwaka (2013-2015).

Alizaliwa mwaka 1990, na sasa anasomea shahada ya uzamili katika masuala ya maendeleo kwenye chuo kikuu cha Colombo alikopata pia shahada yake ya kwanza ya sayansi.