Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lazima tuyafikirie madhila na machungu kwa watoto wakimbizi-Jolie

Lazima tuyafikirie madhila na machungu kwa watoto wakimbizi-Jolie

Lazima dunia ifikirie madhila na machungu wanayopitia watoto wakimbizi hususan wasichana. Wito huo umetolewa leo Jumanne siku ya wakimbizi duniani na mwakilishi maalumu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Angelina Jolie alipowatembelea wasichana wakimbizi mjini Nairobi Kenya.

Bi. Jolie amekutana na wasichana 20 ambao wako peke yao bila wazazi au walitenganishwa na wazazi wao na sasa wanaishi katika kituo cha Heshima mjini Nairobi Kenya na wanashiriki katika programu maalumu ya kuwawezesha wasichana.

Wasichana hao walikimbia vita au mauaji nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Sudan Kusini, Somalia, Burundi na Rwanda. Na karibu wote walipitia ukatili wa kingono, wa kijinsia, na kuporwa utoto wao.

Wengi wao wamejifungua baada ya kubakwa au ni wajawazito, wamemwelezea Jolie hadithi zao za masikitiko na maisha waliyonayo sasa.

Jolie ambaye ameishukuru serikali ya Kenya kwa kuhifadhi wimbi kubwa la wakimbizi amehimiza kwamba jinsi watu wanavyowatendea wakimbizi ni kipimo cha utu wa mataifa yao , huku akisema anapowaona watoto kama wasichana hao, haoni wakimbizi bali anaona binadamu ambao wanateseka sio kwa kupenda kwao bali kutokana na mazingira yaliyo nje ya uwezo wao, hivyo ameiambia dunia kuendelea kushikamana na wakimbizi