Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 1000 wa Sudan Kusini husaka hifadhi kila siku-UNICEF

Watoto 1000 wa Sudan Kusini husaka hifadhi kila siku-UNICEF

Wakati dunia leo ikiadhimisha siku ya wakimbizi, watoto 1000 kila siku hufurushwa makwao kusaka hifadhi nchini Sudani Kusini limsema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF,na kuongeza kuwa sasa mgogoro huo ni janga kwa watoto.

Katika taarifa yake leo, UNICEF imesema tangu kuanza kwa mgogoro huo mwaka 2013, zaidi ya watu miliomni 1.8 wamevuka mpaka kusaka hifadhi nchini Uganda, Ethiopia na Kenya, huku idadi kubwa zaidi kiwa nchini Uganda.

Shirika hilo kadhalika linasema hali katika nchi zinazohifadhi wakimbizi hao ni tete kwani zimezidiwa uwezo, mathalani Uganda ambayo inahifadhi zaidi ya wakimbizi nusu milioni.

Takwimu hizi zinaripotiwa siku mbili kabla ya mkutano wa kimataifa wa mshikamano na wakimbizi mnamo Juni 22 hadi 23 nchini Uganda, ambapo UNICEF imeonya kuwa asilimia 86 ya wakimbizi wote nchini humo ni wanawake na watoto na hivyo kuitolea wito jumuiya ya kimataifa kutoa fedha za usaidizi kwa taifa hilo la Afrika Mashariki ambalo sasa linaongoza kwa idadi kubwa ya uhifadhi wa wakimbizi barani Afrika.