Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 4000 hawana makazi baada ya moto kuteketeza kambi ya Korma Darfur

Watu 4000 hawana makazi baada ya moto kuteketeza kambi ya Korma Darfur

Watu 4, 000 wameachwa bila makazi na sasa wanaishi chini ya miti baada ya moto mkubwa kuteketeza kabisa kambi waliyokuwa wanaishi kwenye jimbo la Darfur nchini Sudan.

Tukio hilo lilitokea Ijumaa kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Korma iliyoko kilometa 80 kutoka El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini, umesema mpango wa Umoja wa Mataifa na muungano wa Afrika wa kulinda amani Darfur, UNAMID.

Moto huo umesambaratisha kabisa majengo ya kambi hiyo yaliyokuwa yanakaliwa na familia 1000. Watu watano wamepoteza maisha pamoja na mifugo mingi ikiwemo ng’ombe, punda na farasi.

Vikosi vya UNAMID vilisaidia kuzima moto huo na kutoa huduma ya kwanza kwa majeruhi. Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada hivi sasa yanatoa msaada wa vifaa muhimu kwa watu hao ikiwemo magodoro ya kulalia, maguduria ya maji na vyombo vya kupikia.