Kamishina Mkuu wa wakimbizi azuru Sudan Kusini-UNHCR

18 Juni 2017

Kamishina mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi amekuwa ziarani nchini Sudan Kusini. Akiwa nchini humo bwana Grandi amezuru eneo la ulinzi wa raia karibu na mji kuu Juba linalohifadhi watu zaidi ya 30,000.

Katika eneo hilo amekutana na kundi la wanawake ambao wametembea kwa juma zima kufika katika eneo hilo. Miongoni mwao ni Sarah aliyemweleza bwana Grandi anataka kumaliza shule lakini hawezi kutokana na sababu za kiusalama . Bwana Grandi amesema anaelewa kuwa hilo ni tatizo na kwamba

(SAUTI YA GRAND)

“Kama hakuna usalama ni kazi bure , na suala la usama ndilo linalotamalaki hapa , hicho ndicho nilichokisia kutoka kwa wakimbizi wa ndani.”

Mwishoni mwa 2016 ilikadiriwa kwamba raia milioni 1.9 wa Sudan Kusini ni wakimbizi wa ndani huku wengine milioni 1.9 wamekimbilia nchi jirani kusaka usalama. Mgogoro huo unakabiliwa na uhaba wa ufadhili huku mashirika ya kibinadamu yakihaha kutoa msaada wa msingi unahohitajika. Grandi anaeleza kwa nini amezuru Sudan Kusini wakati huu

(SAUTI YA GRANDI CUT 2)

‘Nimeamua kuja hapa katika wiki hii ya siku ya wakimbizi duniani kwa sababu nafikiri kwamba mgogoro huu wa wakimbizi unakuwa kwa haraka sana kati ya migogoro ya wakimbizi duniani leo hii, na kwa wote waliotawanywa na wakimbizi."

Kamishina Grandi anasema dhamira ya watu hao ni dhahiri kwa serikali, pande kinzani na jumuiya ya kimataifa , wanachokitaka ni amani. Mwaka 2013 ahadi ya taifa hilo changa kabisa duniani ilianza kutoweka wakati mamilioni ya watu walipolazimika kuzikimbia nyumba zao. Mapigano yanayoendelea baina ya serikali na makundi yenye silaha yanatishia mamilioni ya watu ambao sasa wanakabiliwa na ukame na baa la njaa.