Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Saidieni adha ya maji Yemen kuepusha janga la kipindupindu:UM

Saidieni adha ya maji Yemen kuepusha janga la kipindupindu:UM

Yemen na jumuiya ya kimataifa ni lazima wachukue hatua haraka kutoa maji salama ya kunywa ili kuzuia kusambaa zaidi kwa mlipuko wa kipindupindu, wameonya wataalamu wa haki za binadamu Ijumaa.

Zaidi ya watu 135,000 wanahofiwa tayari wameshapata kipindupindu , wakati taifa hilo bado linakabiliana na vita vinavyoendelea ,ambavyo vimechangia kusambaratika kwa miundombinu ya maji na usafi nchini humo.

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya ulimwenguni WHO , zaidi ya watu 950 wameshafariki dunia na kipundupindu, na maafisa wanahofia kwamba kutakuwa na idadi kubwa zaidi ya vifo kwani ugonjwa unaendelea kusambaa.

Léo Heller,  mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya maji na usafi na Dainius Pûras, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya afya wamewataka wadau wote kuimarisha juhudi za kujenga na kukarabati miundombinu hiyo ili kuhakikisha upatikanaji wa maji ya kunywa na usafi.