Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kitendo cha dharau-UNSOM

Shambulio wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kitendo cha dharau-UNSOM

Nchini Somalia watu wapatao 19 wameuawa baada ya gari lililokuwa na vilipuzi kulipuka kwenye mgahawa wa Pizza na hoteli jirani ya Posh mjini Mogadishu.

Kikundi cha kigaidi cha Al-Shabaab kimekiri kuhusika na shambulio la leo lililolenga wateja waliokwenda kufuturu kwenye mgahawa huo ambapo hata hivyo walinzi wa mgahawa huo waliua wanamgambo watano wa kikundi hicho.

Kufuatia tukio hilo, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Michael Keating amelaani vikali akisema hakuna jambo lolote linaloweza kuhalalisha vitendo hivyo katili vya umwagaji damu.

Amesema mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kipindi cha amani na upendo akisema washambuliaji wameonyesha dharau.

Bwana Keating ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Somalia, UNSOM, ametuma salamu za rambirambi kwa wafiwa na kuwatakia ahueni ya haraka majeruhi.