Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji na wakimbizi wanyanyaswa na kushikiliwa bila ridhaa yao Libya-IOM

Wahamiaji na wakimbizi wanyanyaswa na kushikiliwa bila ridhaa yao Libya-IOM

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limesema linatiwa hofu na hali ya takribani wakimbizi na wahamiaji 260 wa Somalia na Ethiopia wakiwemo watoto wanaoshikiliwa na wasafirishaji haramu wa binadamu au magenge ya wahalifu nchini Libya bila ridhaa yao.

Kwa mujibu wa IOM picha za video zilizosambazwa kwenye mtandao wa kijamii wa facebook Juni 9 zinawaonyesha mamia ya watu hao waliohamanika na kuteswa wakiwa wamekusanywa kwenye chumba kidogo huku wakiwa na hofu kubwa. Inawezekana pia kuna raia wa mataifa mengine.

Wahamiaji na wakimbizi hao wameelezea madhila yanayowasibu ikiwemo kupigwa, kuteswa, wengine hata kutolewa meno, kuvunjwa mikono na kunyimwa chakula.

Wamesema wanawake wametenganishwa na wanahofia huenda wanateswa zaidi na hata kufanyiwa ukatili wa kingono. Wazazi na jamaa wa wakimbizi na wahamiaji hao pia wamekuwa wakitumiwa vipande vya video vya ndugu zao kupitia mitandao ya kijamii na kutakiwa kulipa kati ya dola 8000 hadi 10,000 au jamaa zao watauawa.

Naye mkurugenzi wa UNHCR kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini Amin Awad, amesema shirika hilo linaungana na IOM kutaka kujua mustakhabi wa wakimbizi na wahamiaji hao na kutoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa ushirikiano na serikali ya Libya.