Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu ni haki ya binadamu

Elimu ni haki ya binadamu

Matumaini yetu ni kuelimisha watoto milioni sita duniani kwa kutoa mafunzo kwa walimu milioni moja ifikapo mwaka 2030 kote ulimwenguni. Hiyo ni kauli ya Brian Messenger Afisa Masoko wa kimataifa kutoka shule ya kimataifa ya Perkins iliyoko mji wa Boston jimbo la Massachusetts, Marekani ambayo ni ya watu wenye ulemavu wa macho au wasioona, inayofanya kazi katika nchi arobaini zikiwemo nchi zilizoko Amerika ya Kusini, Afrika, Mashariki ya Kati, Asia na Ulaya.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Idhaa hii kandoni mwa mkutano wa 10 wa nchi wanachama wa mkataba wa haki za watu wenye ulemavu CRPD, Bwana Messenger amesema kumuelimisha mwalimu mmoja ni sawa na kuua ndege wawili kwa jiwe moja.

(SAUTI BRIAN MESSENGER)

“Kutoa mafunzo kwa walimu ndio lengo letu maalum na tumekuwa tunatoa mafunzo kwa walimu kote ulimwenguni tangu 1921, ili kufikia idadi ya watoto wenye mahitaji maalum, njia mujarabu ya kuwafikia ni kupitia mafunzo kwa walimu kwa sababu iwapo utatoa mafunzo kwa mwalimu mmoja atakuwa na fursa ya kubadili maisha ya watoto wengi kupitia kazi zake”

Ameongeza kuwa anatarajia ushirikiano zaidi katika kuhakikisha utimizaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs hususan lengo namba 4 la kuhakikisha fursa za elimu kwa wote.