Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji wawatoa mamilioni katika umasikini kwa kutuma fedha nyumbani

Wahamiaji wawatoa mamilioni katika umasikini kwa kutuma fedha nyumbani

Kiwango cha fedha kinachotumwa na wahamiaji kwa familia zao nyumbani kimeongezeka na kufikia asilimia 51 katika muongo uliopita kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa Jumatano na mfuko wa kimataifa wa ufadhili kwa maendeleo ya kilimo IFAD.

Utafiti umejikita katika kipindi cha miaka kumi ya wahamiaji kutuma fedha nyumbani walikotoka ambacho ni kati ya 2007 hadi 2016. Ripoti inaonyesha kwamba kumekuwa na ongezeko karibu katika kanda zote duniani,  hata hivyo ongezeko hilo limechangiwa zaidi na bara la Asia ambalo pekee limeshuhudia ongezeko la zaidi ya asilimia 87.

Zaidi ya wafanyakazi wahamiaji milioni 200, hivi sasa wanazisaidia familia zao zipatazo milioni 800 kote duniani kwa kuwatumia fedha. Kwa mujibu wa raia wa IFAD Gilbert F. Houngbo kiwango kidogo cha dola 200 au 300 ambacho kila mhamiaji anatuma nyumbani kinaleta mabadiliko makubwa katika maisha ya familia husika. Siku ya kimataifa ya utumaji fedha kwa familia huadhimishwa kila mwaka Juni 16.