Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake bado wana fursa ndogo katika ajira-ILO

Wanawake bado wana fursa ndogo katika ajira-ILO

Pengo la kijinsia limesalia moja ya changamoto inayokabili dunia katika masuala ya kazi, hii ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la kazi duniani ILO inayosema kwamba wanawake wana fursa ndogo zaidi ya kushikiri kwenye soko la ajira ikilinganishwa na wanaume.

Ripoti hiyo iitwayo Ajira duniani na mtizamo wa kijamii- Mwelekeo kwa wanawake 2017, imekwenda mbali zaidi ikisema hata wawapo katika soko la ajira wana fursa ndogo ya kupata kazi na ubora wa kazi yenyewe, na kwamba hili bado ni tatizo.

Mathalani utafiti katika ripoti hiyo umeonyesha kuwa kupunguza na hatimaye kuondoa pengo la kijinsia kazini kwa asilimia 25 hadi mwaka 2025, kwaweza kuongeza hadi dola trilioni 5.8 katika uchumi wa dunia na kukuza mapato yatokanayo na kodi.

Katika muktadha huo wa ajira, ILO katika wavuti wake leo imesema, ukosefu wa ajira duniani kote unatarajiwa kukua kwa asilimi 3.4 milioni kwa mwaka huu wa 2017.