Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Picha mpya za setilaiti kusaidia kubaini baa la nzige

Picha mpya za setilaiti kusaidia kubaini baa la nzige

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema taarifa kutoka setilaiti zinatumika kama njia mpya ya kubaini mazingira bora ya nzige kuzaliana na hivyo kuweza kuchukua hatua mapema kabla wadudu hao hawajashambulia mazao na kusababisha uhaba wa chakula.

Mbinu hiyo ambayo tayari imejaribiwa Algeria, Morocco na Mali, inafuatia ushirikiano kati ya wataalamu wa FAO na wale wa shirika la anga za juu la Ulaya, ESA ambapo wamesema kupitia taarifa hizo wanaweza kutoa onyo miezi miwili kabla ya nzige hao kushamiri.

Mathalani picha hizo za setilaiti zinaangazia unyevunyevu wa udongo na uoto wa kijani wakisema kuwa baa la nzige hutokea wakati wa ukame unapofuatiwa na mvua za kutosha na kasi kubwa ya uoto wa majani.

Mtaalamu kutoka FAO Keith Cressman amesema maonyo ya muda mrefu yanapatia nchi kipindi cha kutosha kuchukua hatua za kuepusha baa la nzige na hivyo kuondokana na hasara iletwayo na wadudu hao.