Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia waendelea kuuliwa, kujeruhiwa Ukarine-UM

Raia waendelea kuuliwa, kujeruhiwa Ukarine-UM

Uvunjifu wa makubaliano ya usitishaji wa mapigano umesababisha kuongezeka kwa idadi ya watu waliokufa kutokana na mgogoro nchini Ukraine, Umoja wa Mataifa umesema leo.

Ujumbe wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu nchini Ukraine (HRMMU), umesema kuwa kati ya Februari na Mei mwaka huu umesajili vifo 36 na majeruhi 157 vitokanavyo na kuendelea kwa mzozo nchini humo.

Katika ripoti ya hivi karibuni ya ujumbe huo iliyopewa jina matumizi ya mara kwa mara ya silaha ndogondogo na makombora mazito, idaidi kubwa ya wahanga wa mgogoro huo wanatoka katika maeneo ya Donetsk na Luhansk nchini humo.

Ripoti imeonya kuwa majira ya kiangazi yanapokaribia, kuna hatari ya kuendelea kwa chuki, inayochochewa na kumiminika kwa wageni na usambazaji wa risasi na silaha nzito.

Tangu kuzuka kwa mgogoro nchini Ukraine mwaka 2014, karibu watu 10,000 wamefariki dunia,wengine zaidi ya milioni 1.6 wamefurushwa huku wengine milioni tatu wakisalia katika maeneo yanayodhibitiwa na vikundi vyenye silaha.