Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali CAR bado tete, MINUSCA iendeleze wito wa amani-Anyanga

Hali CAR bado tete, MINUSCA iendeleze wito wa amani-Anyanga

Baraza la Usalama leo limekutana kujadili hali nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR kama ilivyo katika ripoti nambari (S/2017/473) ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kupitisha ajenda inayohusu CAR.

Katika mkutano wa leo, baraza limeangazia hali ya kiusalama nchini CAR, husuani kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya raia pamoja na wafanyakazi wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, MINUSCA, pamoja na changamoto inayokabili mchakato wa kisiasa.

Akilihutubia baraza la usalama Mwakilishi maalum wa Katibu mkuu nchini CAR Parfait Onanga- Anyanga amesema hali nchini humo inasalia kuwa tete kwani mapigano ya kikabila na kidini yameripotiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi, hususani siku za hivi karibuni.

MINUSCA kwa sasa inahifadhi wakimbizi wa ndani 17,000 huku pia wakimbizi wengine 3,000 waisaka hifadhi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC.

Bwana Anyanga hata hivyo amesema kuna matumaini.

(Sauti Anyanga)

‘‘Hata katikati ya madhila haya, kusambaa kwa vita, adhma yetu inasalia imara kuliko wakati wowote ule. Matokeo yake ni kwamba CAR inasalia katika mwelekeo wa amani.’’