Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ahadi ziende sanjari na vitendo katika kuwahifadhi wakimbizi-Grandi

Ahadi ziende sanjari na vitendo katika kuwahifadhi wakimbizi-Grandi

Wakati mahitaji ya makazi yakiongezeka kimataifa , sanjari na ongezeko la idadi ya wakimbizi, kamishina mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya wakimbizi Filippo Grandi, jumatatu ametoa wito wa kuongeza idadi ya maeneo kwa ajili ya kuhifadhi wakimbizi katika nchi ya tatu.

Kwenye ufunguzi wa majadiliano ya kila mwaka na serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kuhusu makazi ya wakimbizi mjini Geneva Uswis, Grandi amezitaka serikali kote duniani kutenga na kutoa maeneo ya ajili ya wakimbizi kwa kuzingatia azimio la New York lililotiwa saini miezi tisa iliyopita na nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Grandi amesema ukweli ni kwamba mahitaji ya makazi ya wakimbizi ni mengi kuliko maeneo yaliyotengwa na serikali, licha ya nchi nyingi kushiriki katika programu hiyo, sekta binafsi na jamii.

Takribani wakimbizi milioni 1.2 duniani wanahitaji kupatiwa makazi, na maeneo yaliyopo kwa ajili hiyo ni 93,200 pekee ikiwa ni pungufu ya asilimia 43 ya iliyokuwa 2016.