Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majanga na vita ni kichocheo cha utumikishwaji watoto-ILO

Majanga na vita ni kichocheo cha utumikishwaji watoto-ILO

Takriban watoto milioni 168 wahanga wa utumikishwaji wa watoto wanaishi katika maeneo kunakoshuhudiwa vita na majanga. Taarifa kamili na Grace Kaneiya

(Taarifa ya Grace)

Hiyo ni kwa mujibu wa Shirika la kazi ulimwenguni, ILO katika taarifa yake ya siku ya kimataifa ya kupinga utumikishwaji kwa watoto inayoadhimishwa kila mwaka Juni 12.

Maadhimisho ya mwaka huu yamejikita katika athari za vita na majanga kwa utumikishwaji wa watoto wakati takwimu zikionyesha kwamba watu bilioni 1.5 wanaishi katika maeneo kunakoshuhudiwa vita huku watu milioni 200 wakiathirika na majanga kila mwaka, hali ambayo inaathiri maisha yao ya kila siku na kupelekea watu kukosa hudumu za msingi.

ILO imetaja watoto kama waathirika wakubwa wakati kunapozuka vita au majanga kwani mara nyingi shule huhaharibiwa na huduma muhimu hukatizwa na hivyo kusababisha kundi hilo kuwa katika hatari ya biashara ya utumwa na ajira ya utotoni.  Francesco d'Ovidio ni mkuu wa kitengo cha ufumbuzi na utatuzi katika shirika la ILO

(Sauti ya Francesco)

"Ukweli ni kwamba watoto hawa wanayimwa fursa ya kuwa watoto, fursa ya kupata elimu na watakomaa na kuishia kuwa watu wasio na ajira rasmi na hilo litachangia umaskini zaidi  katika nchi na kuzua mzunguko wa matatizo."

Kwa mantiki hiyo jumuiya ya kimataifa imetolewa wito kutokomeza ajira kwa watoto ifikapo mwaka 2025.