Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani 3 wauawa na 8 wajeruhiwa huko Mali

Walinda amani 3 wauawa na 8 wajeruhiwa huko Mali

Walinda amani watatu wa Umoja wa Mataifa wameuawa na wengine wanane wamejeruhiwa katika matukio mawili tofauti huko kidal, kaskazini mwa Mali.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari hii leo kuwa tukio la kwamza lilitokana na kituo cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko Mali, MINUSMA kushambuliwa kwa kombora ambapo walinda amani watano walijeruhiwa.

Amesema kufuatia shambulio hilo MINUSMA ilipeleka timu kufuatilia upande ulikotoka shambulio hilo na ndipo watu wasiojulikana walishambulia eneo la doria kusini mwa kambi ya MINUSCA na kuua walinda amani watatu na wengine watatu wakajeruhiwa.

(Sauti ya Dujarric)

“Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa umelaani mashambulio hayo na kusihi pande husika huko Kidal kusaidia kubaini washambuliaji ili hatimaye wafikishwe mbele ya sheria.”

Bwana Dujarric amesema MINUSMA imetuma salamu za rambirambi kwa wafiwa na kuwatakia ahueni ya haraka majeruhi huku akisema kuwa ujumbe huo umesisitiza azma yake ya kuendelea na operesheni yake ya amani ya kuhakikisha ulinzi wa raia.