Mipango ya kukabiliana na usafirishaji haramu wa binadamu lazima iwe na ufanisi:UM

9 Juni 2017

Biashara nyingi lazima zijitoe kimasomaso kukabiliana na unyanyasaji kazini unaohusiana na usafirishaji haramu wa binadamu amesema mtaalamu wa haki za binadamu Ijumaa.

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa Maria Grazia Giammarinaro, akihutubia baraza la haki za binadamu mjini Geneva Uswis amesema hatua za hiyari zilizopo zinahitaji kufafanuliwa zaidi na ziwe zenye ufanisi.

Kwa mujibu wa shirika la kazi duniani ILO, inakadiriwa kwamba watu milioni 21 ni wahanga wa usafirishaji haramu wa binadamu kote duniani .

Tangu mwaka 2012 mjini California, viwanda vinavyoingiza dola zaidi ya milioni 1000 vinahitajika kusema vinafanya nini kuhakikisha bidhaa zao hazihusiani na utumwa na usafirishaji haramu wa binadamu.

Bi Giammarinaro amesema majimbo mengine pia yanahitaji kufuata nyayo hizo, akiongeza kwamba mikataba itasaidia kuepuka zahma kama ile ya Rana Plaza nchini Bangladesh ambapo zaidi ya wafanyakazi 1000 walipoteza maisha wakati jengo walimokuwa wakifanya kazi lilipoporomoka mwaka 2013.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter