Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkataba wa amani Libya unafanyiwa marekebisho- Kobler

Mkataba wa amani Libya unafanyiwa marekebisho- Kobler

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Martin Kobler amesema hali ya amani nchini humo bado si shwari sana na mwelekeo wa utekelezaji wa mkataba wa amani una nuru kidogo.

Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video kutoka Tunis, Tunisia, Bwana Kobler amesema ingawa kuna muafaka kuwa mkataba wa amani ndio muarobaini pekee wa amani Libya, bado utekelezaji wake haukamiliki.

 (Sauti ya Kobler)

“Nchini Libya bado kipindi cha mpito hakijatekelezwa ipasavyo. Taasisi zinazofanana bado zipo badala ya kuugana. Baraza la wawakilishi halikutambua serikali ya maafikiano ya kitaifa wala halikuridhia marekebisho ya katiba.”

Hata hivyo amesema..

(sauti ya Kobler-2)

“Baada ya miezi ya mashauriano na wadau nchini Libya, wadau wa kikanda na kimataifa, tunaandaa mpango utakaoruhusu marekebisho kidogo ya mkataba wa amani wa Libya kupitia mchakato shirikishi na unaoongozwa na walibya wenyewe.”

Amesema kwa sasa nchini  humo kuna makubaliano ya kwamba suluhu haitopatikana kwa mtutu na kwamba umoja wa Libya unahitaji kuunda serikali moja na yenye taasisi za pamoja za ulinzi.

Bwana Kobler amekumbusha kuwa wananchi wa Libya wana hamu ya amani, usalama na pia wataka mustakhbali bora kwa watoto wao.