Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili dhidi ya watoto washamiri DRC- MONUSCO

Ukatili dhidi ya watoto washamiri DRC- MONUSCO

Jumla ya visa 40 vya ukatili dhidi ya watoto vimeripotiwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kati ya tarehe 29 mwezi uliopita wa Juni na tarehe 5 mwezi huu vikitekelezwa na vikundi vilivyojihami.

Mratibu wa mawasiliano ya umma wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO, Théophane Kinda amewaeleza waandishi wa habari mjini Kinshasa hii leo kuwa idadi hiyo ni sawa na visa vitano kila siku na vimetokea mashariki mwa nchi hiyo.

Ukatili huo kuwa ni pamojana watoto kutumikisha jeshini, ukatili wa kingono na mashambulizi dhidi ya hospitali na shule ambapo vikundi husika ni pamoja na Kamuina Nsapu, Nyatura, Mayi-Mayi Mazembe, Rahiya Mutomboki na M23.

Watoto waliokumbwa na mikasa hiyo wana umri hata chini ya miaka 15 hivyo amesema vitendo hivyo vinaweza kuwa uhalifu dhidi ya kivita kwa mujibu wa mkataba wa Roma.

MONUSCO imesisitiza vikundi hivyo na wanamgambo wao kuzingatia sheria za kimataifa na viache kutumikisha watoto na hivyo wawaachie huru mara moja wale wanaoshikiliwa.