Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu zaidi ya 100,000 kufaidika na msaada wa China Chad:WFP

Watu zaidi ya 100,000 kufaidika na msaada wa China Chad:WFP

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limekaribisha mchango wa kitita cha dola milioni 4 zilizotolewa na Uchina , ambazo zitawapa ahuweni watu zaidi ya laki moja wanaohitaji msaada nchini Chad.

Eneo la ziwa Chad limeghubikwa na machafuko yaliyosababisha mgogoro wa kibinadamu, hivyo mchango huo wa Uchina kwa mujibu wa WFP utaliwezesha shirika hilo kutoa msaada wa chakula kwa watu 57,000, wakiwemo karibu wanawake 30,000 na watoto zaidi ya 100,000 walio na umri wa chini ya miaka mitano Mashariki mwa nchi hiyo.

Pia utakuwa nuru kwa wakimbizi zaidi ya 44,000 wa Sudan Kusini ambao wameishi Chad bila matumaini ya kurejea nyumbani kwa takribani miaka 10. Msaada huo wa kwanza wa Uchina ni ishara ya ushirika mzuri na WFP na pia juhudi za serikali ya Chad za kutimiza lengo nambari mbili la maendeleo endelevu la kutokomeza njaa.