Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usawa wa kijinsia bado ni changamoto katika elimu-UNESCO

Usawa wa kijinsia bado ni changamoto katika elimu-UNESCO

Licha ya hatua kubwa iliyopigwa katika kupanua fursa za elimu, usawa wa kijinsia katika elimu unasalia kuwa changamoto kubwa.

Kwa mujibu wa shirika la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO, wasichana wengi zaidi wako shule hii leo kuliko wakati mwingine wowote, lakini sababu za kijamii, kiuchumi na ubaguzi wa kijinsia zinawazuia wasichana hao kupata fursa sawa ya kumaliza na kufaidika na elimu waliyochagua.

Shirika hilo linasema hofu kubwa ni ushiriki mdogo wa wasichana katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) na ajira katika nyanja hizo. UNESCO inasema STEM inatamalaki katika kila nyanja ya maisha na ni kichocheo cha kufikia malengo ya maendeleo endelevu yaani SDG hapo 2030, na pia kutatua changamoto zilizopo na zinazoibuka.

Sasa UNESCO inalivalia njuga suala hilo kwa kuhakikisha uelewa na umuhimu wa STEM kwa wasichana na kushughulikia sababu zinazoathiri ushiriki wao. Kongamano la kwanza la kimataifa la UNESCO kuhusu elimu ya wasicha katika STEM litafanyika Bankok Thailand Agost 28-30 mwaka huu.