Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nguli Grenier ateuliwa balozi mwema wa mazingira

Nguli Grenier ateuliwa balozi mwema wa mazingira

Mcheza filamu nguli wa Marekani Adrian Grenier, ameteuliwa na mpango wa Umoja wa Mataifa wa mazingira UNEP kuwa balozi mwema wa mazingira. Nguli huyo anatarajiwa kupigia chepuo upunguzwaji wa matumizi ya plastiki na ulinzi wa viumbe vya baharini.

Taarifa ya UNEP kuhusu uteuzi huo inasema kwamba mcheza filamu huyo mashuhuri kadhalika atawashawishi mashabiki wake kuwa makini katika kufanya uamuzi katika kupunguza madhara ya uharibifu wa mazingira.

Akizungumza mjini New York Marekani, baada ya kuteuliwa, Grenier amesema ni muhimu kupigia chepuo umakini na kujitoa katika kufikiria mipango ya mazingira ya kuleta mabadiliko.

Amesema amejiandaa vyema katika kubuni njia mbazo kwazo jamii ya kimataifa yaweza kuja pamoja kusaidia katika kunusuru majanga ya hali ya hewa kwa ushirikiano.