Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia inahitaji "mapinduzi" katika huduma ya afya ya akili:UM

Dunia inahitaji "mapinduzi" katika huduma ya afya ya akili:UM

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa mataifa kuhusu haki ya afya , Dainius Pûras, ametoa wito wa mabadiliko katika huduma ya afya ya akili kote duniani , akizitaka nchi na wataalamu wa afya ya akili kuchukua hatua kwa ujasiri kufanyia mapinduzi mfumo uliokumbwa na mtafaruku ambao umejengeka katika hulka zilizopitwa na wakati.

Akiwasilisha ripoti yake kwenye baraza la haki za binadamu mjini Geneva Jumanne, bwana Pûras amesema kunahitajika mapinduzi hayo kwenye mfumo wa afya ya akili ili kukomesha miongo ya kupuuzwa, unyanyasaji na ukatili .

Ameongeza kuwa afya ya akili inapuuzwa katika mifumo ya afya kote duniani , na kuliko na mifumo ya afya ya akili basi wanatengwa na huduma zingine za afya kwa kuzingatia hulka zilizopitwa na wakati na huo ni ukiukaji wa haki za binadamu..

Amesisitiza ni lazima nchi zichukue mtazamo mpya unaozingatia haki za binadamu katika suala la afya ya akili, akionya kwamba mamlaka na maamuzi kuhusu afya ya akili yako mikononi mwa wataalamu wa afya hususani ya akili, na watalaamu hao wanaungwa mkono na viwanda na makampuni ya dawa hivyo wana wajibu mkubwa kuhakikisha wagonjwa wa afya ya akili wanapatiwa huduma inayostahili kwa kuzingatia haki za binadamu.