Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada kwa ajili ya elimu wapungua mwaka wa sita mfululizo-UNESCO

Msaada kwa ajili ya elimu wapungua mwaka wa sita mfululizo-UNESCO

Kiwango cha fedha za msaada kwa ajili ya elimu kimeporomoka kwa mwaka wa sita mfululizo imesema leo ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO iliyotolewa Jumanne. Taarifa kamili na Flora Nducha.

(Taarifa ya Flora)

Ripoti hiyo ya ufuatiliaji wa elimu kimataifa (GEM) iitwayo “Msaada kwa elimu unadorora na kutowafikia wanaouhitaji zaidi” inasema jumla ya dola bilioni 12 ndio zilizofadhili elimu mwaka huu hadi sasa ikiwa ni asilimia 4 chini ya ilivyokuwa mwaka 2010 ambapo msaada huo ulikuwa na ongezeko la asilimia 24.

Kwa mujibu wa Irina Bokova mkurugenzi mkuu wa UNESCO msada wa fedha ni mdogo kuliko mahitaji ya kuweza kufikia lengo la maendeleo endelevu nambari 4 linalohusu elimu. Amesema maeneo ambayo yanaguswa zaidi ni elimu ya awali, elimu ya msingi, elimu ya sekondari na elimu ya watu wazima.

Ripoti hiyo inapendekeza mambo matatu, mosi kampeni ya kuchangisha dola bilioni 3.1 kati ya 2018-2020, pili kuwa na kitengo cha kimataifa cha fedha kwa ajili ya ufadhili wa elimu na tatu wakfu wa "Elimu haiwezi kusubiri" ulioanzishwa mwaka 2016 utaweza kuchangisha dola bilioni 10 za ziada kila mwaka ifikapo 2020.