Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 15 wafariki dunia baada ya chanjo ya surua kwenda mrama Sudan kusini

Watoto 15 wafariki dunia baada ya chanjo ya surua kwenda mrama Sudan kusini

Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema limesikitishwa na taarifa ya vifo vya watoto 15 katika kijiji cha Nachodokopele Mashariki mwa Kapwete nchini Sudan Kusini, vinavyohusiana na kampeni ya chanjo ya surua ya tarehe 10 hadi 14 Mei kwenda mrama.

Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa Alhamisi na WHO, shirika la kuhudumia watoto UNICEF na wizara ya afya ya Sudan Kusini ,baada ya uchunguzi wa kina wa vifo hivyo imebainika kwamba kampeni hiyo ya chanjo ilihusika na vifo hivyo kama anavyofafanua Tariki Jasarevic msemaji wa WHO

(SAUTI YA TARIK)

“Kwa mujibu wa ripoti makossa ya kibinadamu yamechangia vifo hivyo ambayo ni matumizi ya wahudumu wasio na ujuzi na mafunzo ya uelewa wa jinsi ya kutoa chanjo kwa viwango vinavyotakia na kutofuatilia na kusimamia ipasavyo utoaji chanjo hiyo.”

Ameongeza kuwa bomba moja la sindano lilitumika kutoa chanjo kwa siku zote nne badala ya kutupwa baada ya kutumika mara moja jambo ambalo ni kinyume na viwango vya afya na usalama vya WHO, na kusababisha dawa ya chanjo kuchanganyika na vitu visivyotakiwa na kuwadhuru watoto.