Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunahitaji kuimarisha usimamizi wa bahari:Thomson

Tunahitaji kuimarisha usimamizi wa bahari:Thomson

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Peter Thomson amesema umuhimu wa uchumi wa bahari endelevu ni dhahiri hasa katika maeneo ya pwani ya Afrika na bara zima kwa ujumla na kuwa wakati umewadia kwa nchi zote kutimiza kwa uadilifu lengo namba 14 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Thomson amesema hayo wakati wa mahojiano na Idara ya Habari ya Umoja wa Mataifa kuelekea mkutano wa kimataifa kuhusu masuala ya bahari utakaoanza wiki ijayo.

Lengo la mkutano huo ni kubaini namna ya kusaidia utekelezaji na kufikia lengo hilo mwaka 2020 au 2030??? , kujadili mafanikio yaliyopatikana hadi sasa na kujenga ushirikiano baina ya wadau mbalimbali.

Amesema wakati wa ziara yake barani Afrika, ujumbe mkubwa alioupata kutoka kwa serikali na jamii za wavuvi ni kwamba wanataka mkutano huo ufanikiwe hususan katika suala la kuleta usimamizi mzuri wa hifadhi ya samaki, na kuratibu wavuvi wa viwanda vikubwa wanaoingia na kumaliza samaki katika maeneo yao asili ya uvuvi.

Vile vile amegusia suala la mabadiliko ya tabianchi ambayo yatajadiliwa katika mkutano huo kuhusu bahari akisema hizo zote mbili ni sarafu moja yenye pande tofauti, na hivyo ..

(Sauti ya Thomson)

"Ni lazima tuimarishe kile kinachoendelea katika Mkataba wa Paris kuhusu tabianchi, kile tunachokifanya katika sayansi nzuri, kuhusiana na hatua kuhusu hali ya hewa, na kuhamishia hilo katika kupambana na tatizo la tindikali baharini, ongezeko la joto la bahari, na kupungua kwa hewa ya oksijeni baharini, na hilo litakua moja ya mafanikio mengine makubwa kwetu sisi"