Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa siku za uvuvi haramu zahesabiwa- FAO

Sasa siku za uvuvi haramu zahesabiwa- FAO

Harakati za kutokomeza uvuvi haramu zinazidi kung’ara baada ya Japan na Montenegro kutia saini mkataba wa kimataifa wa kudhibiti uvuvi huo.

Makubaliano hayo yaitwayo Port State Measures , au PSMA yanahusisha zaidi ya theluthi mbili za sekta ya uvuvi duniani yakileta pamoja nchi wanachama zipatazo 50.

PSMA imeundwa kuzuia meli za uvuvi kujihusisha na uvuvi haramu ambao thamani yake kwa mwaka kwa mujibu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO ni dola bilioni 23.

Mathalani meli za uvuvi zisizokidhi kanuni ikiwemo kuwa na leseni sahihi na kutangaza aina na kiwango cha samaki kilichovulia, hazitaruhusiwa kutia nanga bandarini.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO José Graziano da Silva amekaribisha mkataba huo akisema kuwa ni ahadi ya kuimarisha uhakika wa chakula miongoni mwa jamii za pwani na pia kupunguza shughuli za uvuvi haramu.