Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusipomakinika viumbe hai watatoweka

Tusipomakinika viumbe hai watatoweka

Hatuwezi kufurahia haki zetu za msingi za kibinadamu bila ya mazingira bora, huo ni ujumbe wa Mtaalamu Huru wa Haki za Binadamu kuhusu Mazingira, John H. Knox katika kuelekea Siku ya Mazingira Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Juni 05.

Amesema wanasayansi wanahofu kwamba kwa mara ya kwanza katika miaka milioni 60, ulimwengu umo mwanzoni mwa awamu ya sita ya kutoweka kwa uhai kwani uhai wetu ambao ni lishe, malazi, mavazi, hewa na maji unategemea mfumo bora wa ekolojia, ambao sasa unatokomea kwa kasi kubwa.

Halikadhalika amesema karibu theluthi moja ya asili na urithi mchanganyiko wa ulimwengu vinakabiliwa na ujangili, ukataji miti na uvuvi haramu unaohatarisha zaidi maisha ya viumbe waliohatarini kutoweka na jamii inayotegemea ustawi wake.

Knox amesema kuwa viumbe hai na haki za binadamu vinakwenda sambamba, hivyo mataifa yatekeleze ahadi zao na kutimiza wajibu wao wa kisheria katika kulinda ulimwengu, viumbe hai vyake na wale wanaotetea uhai wake.