Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sheria mpya Misri yakandamiza mashirika ya kiraia- Zeid

Sheria mpya Misri yakandamiza mashirika ya kiraia- Zeid

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein ametaka serikali ya Misri ifute sheria mpya kuhusu utendaji wa mashirika yasiyo ya kiserikali nchini humo akisema ni kandamizi.

Amenukuliwa na ofisi ya haki za binadamu akisema kuwa sheria hiyo namba 70 ya mwaka 2017 inabinya nafasi ya haki za binadamu kwa kuwa inazuia uwezo wa mashirika hayo kufuatilia utendaji wa serikali na kuripoti bila kusahau kupata usaidizi wa kifedha kutoka nje ya nchi.

Bwana Zeid amesema sheria ya sasa ni mwendelezo wa sheria ya awali ya mwaka 2002 iliyosababisha kufutwa kwa mashrika ya kiraia ambayo amesema wajibu wao ni kuwajibisha serikali na hivyo ni lazima yapatiwe uwezo kisheria.

Kamishna huyo ameisihi serikali ya Misri kwa kushirikiana na mashirika ya kiraia wasake mwelekeo mpya kwa maslahi ya raia.