Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM inafanya uchunguzi Kakuma na Dadaab Kenya

IOM inafanya uchunguzi Kakuma na Dadaab Kenya

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM limesema Alhamisi linafanya uchunguzi dhidi ya shutuma za utovu wa nidhamu katika kambi za wakimbizi za Kakuma na Dadaab nchini Kenya.

Ofisi ya mkaguzi mkuu wa IOM ndio inayoendesha uchunguzi huo ikihusisha timu ya wataalamu wa upelelezi.

Na endapo uchunguzi huo utathibitisha kuwepo kwa utovu wa nidhamu kwa IOM au wafanyakazi wake , shirika hilo limesema mkurugunzi mkuu wa IOM William Lacy Swing anajiandaa kuchukua hatua zinazohitajika.

Bwana Swing amesema shirika hilo lina sera ya kutovumilia ukiukwaji wowote wa sheria na utovu wa nidhamu na kipaumbele chake ni kuhakikisha usalama na kuwalinda wahamiaji wasiojiweza hivyo pia shirika hilo litafanya tathimini ya uongozi na operesheni zake katika kambi zote mbili.