Kuna matumaini CAR sasa ukilinganisha na 2014-Gilmour

Kuna matumaini CAR sasa ukilinganisha na 2014-Gilmour

Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR ya mwaka 2014 iliyoghubikwa na hofu, machafuko, mauaji, kuporomoka kwa uchumi na zahma ya kibinadamu, sio CAR ya sasa inayotia matumaini.

Kauli hiyo imetolewa na Andrew Gilmour msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu haki za binadamu ambaye amehitimisha ziara ya siku nne nchini humo.

Bwana Gilmour amesema ameshuhudia kuimarika kwa usalama katika mji mkuu Bangui, soko likishamiri na kutoa ishara ya kukua kwa uchumi, huku polisi na taasisi za kisheria na uongozi wa taifa hilo vikianza kupata taswira mpya, hasa katika kuhakikisha haki kwa wote na kukomesha ukwepaji wa sheria. Hivyo ameongeza..

(SAUTI YA GILMOUR)

"Ili kufungua ukurasa mpya, na kupiga hatua kuelekea amani na maridhiano, kunahitajika uwepo wa haki. Na ripoti hii itachangia hilo. Kuna mahakama ya uhalifu maalum ambayo imeanzishwa na mwendesha mashatka amewasili na kwa hakika ripoti yetu itakuwa muhimu kwake na mahakama itasongesha mchakato wa haki kwakila mtu."