Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hofu juu ya maisha ya watoto walio kwenye nyumba za malezi- UNICEF

Hofu juu ya maisha ya watoto walio kwenye nyumba za malezi- UNICEF

Shirika Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema bado kuna pengo kubwa juu ya idadi halisi ya watoto wanaoishi kwenye makazi ya malezi.

Katika ripoti yake hii leo, UNICEF imesema takwimu kutoka nchi 140 imeonyesha kuwa takribani watoto milioni 2.7 wanaishi katika nyumba hizo za malezi au familia za ulezi maeneo mbali mbali ulimwenguni, idadi ambayo inaonekana kuwa ni ndogo kuliko inavyodhaniwa.

Cornelius Williams ambaye ni mkurugenzi msaidizi wa ulinzi wa watoto UNICEF amesema wamebaini kutokuwepo kwa mfumo makini wa ukusanyaji takwimu kuhusu watoto wakati huu ambapo watoto wanaripotiwa kukimbia mizozo na ghasia makwao.

Amesema watoto hao ambao hawajulikani waliko wako hatarini zaidi kukumbwa na ukatili na hivyo maendeleo yao kiakili na kimwili yanaweza kudumazwa.

Alex Neculai ni mmoja wa watoto ambao wanaishi na familia huko Romania baada ya maisha kwenye familia yao kuwa magumu.

(Sauti ya Alex)

“Wakati Valerica na Horje walipokuja nyumbani, hatukufahamu wamefuata nini. Emmanueli na mimi tulikuwa tumechoka sana. Hatukufahamu na ilituchukua kama wiki nzima kuzoea na kupenda makazi mapya.”

UNICEF inasema ni muhimu serikali kuweka orodha ya kina kuhusu huduma kwenye nyumba za malezi ya watoto na pia kufuatilia watoto wanaoishi kwenye makazi hayo ili kusaidia kuimarisha takwimu.

image
Mtoto Florica, mwenye umri wa miaka 15, akitumia jokofu kama meza ya kufanyia kazi yake ya shule. Florica anaishi Buhusi, jimbo la Bacau nchini Romania. (Picha:.© UNICEF/UN039016/Dinulescu)