Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 3 zaidhinishwa kusaidia janga la kibinadamu Kasaï

Dola milioni 3 zaidhinishwa kusaidia janga la kibinadamu Kasaï

Mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRc Mamadou Diallo ameidhinisha kiasi cha dola milioni Tatu kwa ajili ya usaidizi wa kibinadamu kwenye majimbo yaliyoko ukanda wa Kasaï nchini humo.

Dkt. Diallo ambaye pia ni Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko DRC, amesema pesa hizo zinalenga majimbo ya Kasaï , Kasaï Kati na Kasaï Mashariki ambako mapigano kati ya jeshi na vikundi vilivyojihami yamesababisha adha ya kibinadamu kwa wananchi.

Huduma lengwa ni kama vile afya ya msingi na lishe bora kupitia mipango inayoendeshwa na mashirika mbalimbali likiwemo shirika la mpango wa chakula duniani, WFP.

Nchini DRC watoto milioni 3.5 wanakabiliwa na utapiamlo ilhali kati yao hao, milioni 1.9 wanakabiliwa na utapiamlo uliokithiri au unyafuzi.