Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yataka serikali zichukue hatua dhidi ya uziwi

WHO yataka serikali zichukue hatua dhidi ya uziwi

Mkutano wa 70 wa baraza la afya la shirika la afya ulimwenguni, WHO umefunga pazia hii leo huko Geneva, Uswisi ambapo pamoja na mambo muhimu yaliyopitishwa ni azimio kuhusu kuimarisha hatua dhidi ya uziwi na kupoteza uwezo wa kusikia.

Wajumbe kutoka nchi 194 wanachama wa WHO wamesema wamechukua hatua hiyo kwa kuzingaitia kuwa watu wapatao milioni 360 kote ulimwenguni wanakabiliwa na uziwi, miongoni mwao milioni 32 ni watoto na milioni 180 ni watu wazima wengi wakiwa katika nchi za vipato vya chini na kati.

Kupitia azimio hilo WHO inataka serikali kujumuisha katika huduma ya afya ya msingi masuala ya matibabu na kinga dhidi ya uziwi kwa kutumia mbinu rahisi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Margaret Chan katika hotuba yake ya kufunga baraza hilo amesema..

(Sauti ya Dkt. Margaret)

“Uwekezaji katika afya unatoa matokeo ya kipekee na yanayopimika, halikadhalika ni kama mkakati wa kupunguza umaskini.”