Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yawaripoti polisi wafanyakazi wake Kenya kwa udanganyifu Kakuma

UNHCR yawaripoti polisi wafanyakazi wake Kenya kwa udanganyifu Kakuma

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linachukua hatua kadhaa ili kuimarisha uongozi na usimamizi wa operesheni zake katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya baada ya uchunguzi wa ndani kubaini kuna udanganyifu na utovu mkubwa wa nidhamu.

Uchunguzi huo wa UNHCR ulichochewa na shutuma zilizopokelewa za udanganyifu, ufisadi na vitisho kambini na kisha kuthibitisha wafanyakazi watano kuhusika na vitendo hivyo, ambapo sasa hatua kadhaa zimechukuliwa.

Hatua hizo ni pamoja na ofisi ya masuala ya kisheria ya Umoja wa Mataifa kuzipeleka kesi tatu kwa polisi wa Kenya kwa ajili ya mashitaka ya jinai. Hadi sasa mtu mmoja amekamatwa, wafanyakazi wawili kati ya watano wamejiuzulu na mchakato wa hatua za kinidhamu unaendelea dhidi ya wafanyakazi watatu waliosalia.

UNHCR pia imeanzisha tathimini huru ya uongozi wake Kakuma na kuwajulisha washirika wake na wahisani Kenya na Geneva kuhusu kisa hicho na uchunguzi unaoendelea.