Hebu legezeni masharti misaada ifikie walengwa Syria- - O’Brien

30 Mei 2017

Sikuja hapa leo kusaka upendeleo! Ni sehemu ya hotuba ya mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu, OCHA, Stephen O’Brien wakati akihutubia Baraza la Usalama hii leo kuhusu hali Mashariki ya Kati, wakiangazia zaidi Syria.

O’Brien amesema badala yake anawapatia wajumbe wa Baraza hilo hali halisi ya kibinadamu ambayo inazidi kuwa mbaya kila uchao na anachotaka yeye ni kutoa wito ili wahudumu wa misaada ya kibinadamu waruhusiwe bila vikwazo kufikisha misaada hiyo.

“Kutoa wito kwa pande zote kwenye mzozo kulinda raia na miundombinu si kutaka upendeleo. Kutaka watoto wasifukiwe kwenye malundo ya vifusi au chini ya majengo, na kwenye shule si kwamba nabembeleza upendeleo! Dawa kwa wagonjwa na chakula kwa wenye njaa si upendeleo.”

Bwana O’Brien amesema mahitaji hayo ni ya msingi na ambayo ni kwa mujibu wa maadili ya kibinadamu hivyo amesihi wale wote wenye ushawishi na pande kwenye mzozo Syria kuwasisitizia ujumbe huo.

Amesema makubaliano ya Astana yanaonyesha kuzaa matunda ya sitisho la mapigano hivyo amesema ni vyema kuimarisha ushawishi ili makubaliano hayo yaliyoratibiwa na Iran, Urusi na Uturuki yaweza kuendelea kuzingatiwa.

Mzozo wa Syria sasa umeingia mwaka wa saba, miundombinu ya kijamii imesambaratika ambapo licha ya kusababisha vifo na ukimbizi wa ndani na nje, watoto zaidi ya milioni 1.7 hawako shuleni.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter