Mabadiliko ya tabianchi hayana mjadala, shiriki au usalie nyuma: Guterres

30 Mei 2017

Treni endelevu ishang’oa nanga , panda twende au usalie nyuma. Huo ni ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwa viongozi wa dunia kuhusu suala la mabadiliko ya tabia nchi.

Akizungumza Jumanne kwenye kitivo cha biashara katika chuo kikuu cha New York (NYU) kuhusu kuichagiza duniani kuchua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi Guterres, amesema wale watakaoshindwa kukumbatia uchumi unaojali mazingira basi wataishi katika mustakhbali ulioghubikwa na kiza akiongeza kwamba

(GUTERRES CUT 1)

“ Ni muhimu dunia kutekeleza mkataba wa Paris na tukatimiza wajibu wetu kwa malengo. Mabadiliko ya tabia nchi hayana mjadala, hatua dhidi ya mabadiliko hayo hazizuiliki, na suluhu ya mabadiliko ya tabia nchi inatoa fursa ambazo hazilinganishwi.”

Guterres amesema enadapo serikali yoyote duniani itashuku nia ya kimataifa kwa ajili ya mkataba wa Paris basi hiyo ni sababu ya wengine wote kuungana na kuwa imara zaidi, akiongeza kwamba biashara inayojali mazingira ni biashara nzuri , na wale wanaokumbatia teknolojia inayojali mazingira watakuwa wanaweka viwango muafaka vya uongozi katika karne ya 21. Hivyo akasisitiza

(GUTERRES CUT 2)

“Sayansi iko bayana ushawishi wa binadamu katika mabadiliko ya tabia nchi uko wazi, jinsi tunavyozidi kuharibu hali ya hewa ndivyo vinavyoongeza hatari ya kuwa na athari kubwa na zisizoweza kubadilishwa.”

Amesema hatua zikichukuliwa sasa dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi basi kuna fursa kubwa ya amani na mafanikio.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter