Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siwezi kuwaficha hali Yemen haina matumaini yoyote- Ahmed

Siwezi kuwaficha hali Yemen haina matumaini yoyote- Ahmed

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo wamejulishwa kwamba hakuna dalili zozote za kumaliza kwa mzozo nchini Yemen, mzozo ambao licha ya kusababisha vifo, pia umesababisha njaa na magonjwa.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed amesema hayo wakati akihutubia Baraza hilo lililokutana kujadili hali ya Mashariki ya Kati na kuangazia zaidi Yemen, wakati huu ambapo makombora yanazidi kurushwa hasa magharibi mwa jimbo la Taiz.

Bwana Ahmed amesema hawezi kuwaficha wajumbe hao kuwa hakuna nuru ya kupata suluhu Yemen kwa kuwa pande kinzani hazijaonyesha nia ya kuafikiana huku janga la njaa linalosababishwa na binadamu likiacha watu bila chakula.

Hata hivyo amepongeza hatua ya Benki ya Dunia, shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF na taasisi nchini Yemen ya kuanza tena kutoa mgao wa fedha kwa familia maskini zaidi nchini humo akisema..

(Sauti ya Ahmed)

“Ninaamini mpango huo una athari chanya hii leo kwa maisha ya raia wa Yemen.”

Mjumbe huyo maalum akarejelea wito wake..

(Sauti ya Ahmed)

“Kusitasita kwa pande muhimu husika kukubali suala la kulegeza misimamo kwa ajili ya amani, au hata kuyajadili, kunasababisha wayemen walipe gharama kwa vitendo hivyo vya kuchelewa bila sababu yoyote. Natoa wito kwa pande zote kushirikiana na Umoja wa Mataifa bila kuchelewa.”