Maoni ya Katibu Mkuu wa UM Antonio Guterres kuhusu ulinzi wa amani

29 Mei 2017

Nilipoingia jengo la Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa kama Katibu Mkuu wa umoja huo mwezi Januari mwaka huu, jambo la kwanza nililofanya lilikuwa ni kuweka shada la maua kwa heshima ya walinda amani 3,500 waliofariki dunia wakihudumu kwa ajili ya amani. Wiki hiyo hiyo baadaye, walinda amani wawili waliuawa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambako walikuwa na jukumu la kuzuia makabiliano yaliyokuwa yamegubikwa na ghasia kati ya jamii, yasigeuke kuwa mauaji ya halaiki. Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kila siku wanakuwa katika mazingira hatari kati ya vikundi vilivyojihami ambavyo vinajaribu kuuana au kudhuru raia.

Kwa kipindi cha miaka 70 maisha mengi yameokolewa, familia nyingi zilizokumbwa na vita zimepatiwa mwanzo mpya. Utafiti huru umedhihirisha thamani ya ulinzi wa amani: Unazuia kuenea kwa ghasia; unapunguza idadi ya raia wanaouawa kwa asilimia 90 ikilinganishwa na kabla ya kupelekwa kwa vikosi vya ulinzi wa amani.

Tunafahamu pia ya kwamba ulinzi wa amani ni gharama nafuu. Bajeti ya ulinzi wa amani ya Umoja wa Mataifa ni chini ya nusu ya asilimia 1 ya matumizi ya kijeshi duniani. Kiwango hicho kinachangiwa na nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa. Tafiti nchini Marekani zinaonyesha kwamba operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa zina gharama nafuu mara 8 zaidi kuliko pale Marekani inapochukua hatua peke yake. Mara nyingi uwekezaji huu unalipa pindi tunapoangalia ukuaji wa kiuchumi na ustawi unaofuatia baada ya kuongezeka kwa utulivu na usalama kufuatia operesheni za ulinzi wa amani zenye mafanikio.

Katika dunia yetu ya sasa iliyounganika, kuibuka kwa ugaidi kwamaanisha ukosefu wa utulivu popote pale ni tishio kila pahala. Operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa ziko mstari wa mbele katika jitihada zetu za kuzuia kuibuka kwa maeneo yasiyo na utawala wa kisheria, ambako ukosefu wa usalama, uhalifu unaovuka mipaka na misimamo mikali vinaweza kushamiri. Operesheni hizi ni uwekezaji kwa ajili ya amani, usalama na ustawi duniani.

Operesheni zetu zimechangia utulivu, maendeleo na ukuaji wa kiuchumi kuanzia El Salvador hadi Namibia, na kuanzia Msumbiji hadi Cambodia. Operesheni 54 zimekamilisha majukumu yake na zimefungwa.; nyingine mbili huko Liberia na Cote d’Ivoire, zitafanya hivyo miezi michache ijayo.

Wakati Umoja wa Mataifa unakabiliwa na changamoto na vikwazo katika operesheni za ulinzi wa amani, tunapaswa pia kutambua mafanikio ya operesheni hizo za amani.

image
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko Cote D'Ivoire, UNOCI ukikabidhi shule Leban :Picha na UNOCI

Jamhuri ya Afrika ya Kati ilikabiliwa na tishio la kutumbukia kwenye mauaji ya halaiki pindi walinda amani wetu walipowasili miaka miwili iliyopita. Hii leo, nchi hiyo imechagua serikali mpya kupitia mchakato tulivu wa kidemokrasia na inahaha kusongesha amani na utulivu, kupokonya silaha na na kusimamia utawala wa sheria. Operesheni yetu nchini humo, MINUSCA, inatoa msaada muhimu kupunguza vitisho kutoka vikundi vilivyojihami, lakini bado kuna changamoto. Inatia hofu kufikiria madhara ya kutisha ambayo yangalitokea iwapo walinda amani wasingalikuwepo.

Nchini Sudan Kusini, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanahifadhi raia 200,000 ambao walikimbia makazi yao yaliyoharibiwa kufuatia mapigano. Wakati njaa kali inanyemelea nchi hiyo, walinda amani wanawapatia ulinzi wahudumu wa mashirika ya misaada ya kibinadamu ili waweze kufikisha misaada ya kuokoa maisha.

Katika dunia yetu, amani inaonekana kama jambo lisiloweza kamatika. Lakini amani duniani inategemea kazi ngumu tena ya kila siku katika mazingira magumu na hatarishi. Dunia inategemea walinda amani wa Umoja wa Mataifa wafike maeneo ambako wengine hawawezi kufika na hawatafika, licha ya vikwazo vingi ambavyo wanalazimika kukabiliana navyo.

Mara nyingi, operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa hukabiliwa na pengo kati ya malengo yetu na njia za kuyafanikisha. Katika maeneo mengi, walinda amani hupelekwa maeneo ambako pande kinzani huonyesha nia finyu sana ya kuzingatia amani. Operesheni zetu zenyewe zinazidi kulengwa na pande kinzani kwenye mzozo na vikundi vyenye misimamo mikali.

Kushughulikia uhalisia huu wa sasa kunahitaji mkakati wa kina wa marekebisho kwa upande wetu, kwa kuzingatia uchambuzi wa mamlaka zetu na uwezo wa operesheni hizo na ubia wetu na serikali na wengineo. Operesheni zetu za amani zinapaswa kuendana na mazingira hatarishi ambayo wanakabiliwa nayo.

Tayari tumeshafanya marekebisho ambayo yamepunguza kwa kiasi kikubwa gharama na kutupatia uwezo mkubwa wa kupeleka walinda amani ndani ya muda mfupi. Hata hivyo bado kuna mambo mengi ya kufanya. Nimeazimia kushirikiana na serikali, mashirika ya kikanda na wadau wengine kuhakikisha ulinzi wa amani una vifaa na kanuni inazohitaji.

Katika miaka ya karibuni, operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa zimechafuliwa kutokana na visa vya kusikitisha vya ukatili wa kingono na unyanyasaji ambao ni ukiukwaji wa kila kitu ambacho tunakithamini. Kushughulikia janga hili ni kipaumbele cha mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa.

Nimewasilisha mbele ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mpango wenye lengo la kutokomeza ukwepaji sheria. Halikadhalika kwenye ofisi za operesheni zetu za ulinzi wa amani, nitaanzisha nafasi ya mtetezi wa haki za waathirika wa ukatili huo, na pia kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.Nimenuia kuhamasisha viongozi wa dunia katika hatua hizi muhimu.

Watu kote duniani wanapoulizwa kuhusu vipaumbele vyao, kuanzia New York hadi  New Delhi, kutoka Cairo hadi Cape Town, wote wana jibu linalofanana. Wanataka amani na usalama, kukuza watoto wao kwenye mazingira ya amani na kuwapatia elimu na fursa za kuweza kupanga mustakhbali wao.

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa ni mojawapo ya njia ambazo kwazo tunakidhi matarajio hayo ya wakazi wa dunia na kufanya dunia kuwa pahala salama kwa kila mtu.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter