Ulinzi wa amani wasalia jibu la amani ya kudumu ulimwenguni- Guterres

29 Mei 2017

Leo ni siku ya walinda amani duniani ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ulinzi wa amani unasalia kuwa gharama inayoleta unafuu kwa wengi hususan wananchi ambao mizozo husababisha vifo na upotevu wa mali.

Katika maoni yake aliyochapisha kwenye gazeti la Boston Globe la Marekani hii leo, Katibu Mkuu amesema kuwa ingawa bado operesheni hizo zinakumbwa na changamoto bado mafanikio yatokanayo na uwepo wao hayawezi kupingwa.

Amesema kwa miaka 70, operesheni zimeleta manufaa kuanzia Msumbiji hadi El Salvador, Cambodia hadi Namibia, faida ambazo zimesababisha ukuaji wa uchumi na nuru kwa wananchi.

image
Mlinda amani wa UNAMID aizungumza na mama wakati akipiga doria katika kambi ya Zam Zam karibu na El Fasher, Darfur Kaskazini.(Picha:UNAMID/Hamid Abdulsalam)

Hata hivyo amezungumzia kashfa za ukatili wa kingono ambazo zimechafua jina la ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa akisema tayari amechukua hatua ambazo kwazo pamoja na kuepusha ukwepaji sheria, pia zitaleta nuru kwa waathirika wa visa hivyo.

Amesisitiza kuwa gharama ya ulinzi wa amani unaofanywa na Umoja wa Mataifa ni nafuu kuliko nchi moja moja inapoamua kuchukua hatua za ulinzi, akisema bajeti ya mwaka ni chini ya nusu ya asilimia moja ya matumizi ya kijeshi duniani.

Bwana Guterres amesema kote duniani wakati wanataka amani na hivyo ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa ndio unaoweza kukidhi kiu hicho cha wakazi wa dunia.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter