Kipindupindu Yemen chaendelea kuwa mwiba

25 Mei 2017

Nchini Yemen idadi ya watu wanaodhaniwa kuwa wamefariki dunia kutokana na magonjwa ya kuhara na kipindupindu imefikia 418.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia wanahabari jijini New York, Marekani kuwa vifo hivyo ni kati ya visa shukiwa 42,000 vilivyoripotiwa hadi juzi jumatatu.

Amesema ugonjwa unaenea kwa kasi ambapo hadi sasa majimbo 19 kati ya 22 nchini Yemen yana visa vya kuhara au kipindupindu.

Bwana Dujarric amesema kwa kasi ya sasa ya kusambaa kwa magonjwa hayo na ukosefu wa huduma za maji safi na kujisafi, inakadiriwa kuwa ndani ya miezi sita, wagonjwa wapya 100,000 wanaweza kuripotiwa.

Akizungumzia miundombinu ya afya, msemaji huyo ameeleza kuwa ni nusu ya vituo vya huduma ya afya ndio vinafanya kazi Yemen wakati huu ambapo tangu Mei Mosi mwaka huu watu milioni 1.6 wanapatiwa usaidizi wa maji safi na salama na huduma za kujisafi.

Umoja wa Mataifa umepongeza nchi ambazo zimetekeleza ahadi kufuatia mkutano wa usaidizi kwa Yemen huku ukikaribisha mchango mpya wa Marekani wa dola milioni 77 na ule wa Muungano wa Ulaya wa dola milioni 4.3 halikadhalika Norway dola milioni 1.2 kusaidia Yemen.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter