Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tukiokoa riziki tutaokoa pia maisha-FAO/WFP

Tukiokoa riziki tutaokoa pia maisha-FAO/WFP

Wakuu wa mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la mpango wa chakula duniani, WFP na la chakula na kilimo, FAO wametoa wito kwa wadau wa mapigano nchini Sudan Kusini kusitisha uhasama haraka na kuruhusu mashirika hayo kupeleka misaada ya chakula na vifaa vingine kuokoa maisha ya watu milioni 5.5 walio hatarini kukumbwa na njaa kali.

José Graziano da Silva wa FAO na David Beasley wa WFP wametoa wito huo katika jimbo la Unity wakati wa ziara yao nchini humo, eneo ambalo ndilo limeathirika zaidi na baa la njaa, wakitahadhari kuwa msimu wa mwambo unaonza Julai utahatarisha maisha ya watu milioni moja ambao wanakumbwa na baa la njaa.

Hivyo wamesisitiza hatua mseto za usaidizi, itakayochanganya msaada wa dharura wa chakula lakini pia uwezeshaji kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.

Wamesema ingawa vikwazo ni vikubwa, bado kuna uwezekano wa kupunguza vifo na kuepukana na janga la njaa.