Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia itafaidika ikishirikiana na Afrika-Guterres

Dunia itafaidika ikishirikiana na Afrika-Guterres

Watu wote duniani watafaidika endapo watasikiliza, kujifunza na kushirikiana na Afrika. Hiyo ni sehemu ya ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika siku ya Afrika ambayo kila mwaka huadhimishwa Mei 25. Flora Nducha na taarifa kamili (TAARIFA YA FLORA) Guterres amesema siku hii imekuja katika wakati muhimu ambapo bara hilo lipo katika mchakato wa kudumisha amani, kukuza uchumi wake na utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu (SDG’s) sanjari na kwingineko duniani. Ameongeza kuwa Afrika ina mchango mkubwa hasa katika vikosi vya ulinzi wa amani vya Umoja wa Mataifa , lakini pia ni moja ya bara lenye ukarimu duniani kwa kuhifadhi wakimbizi, huku akisisitiza kwamba mipango ya kimataifa ya kutokomeza umasikini, kutokuwepo usawa na haki ni lazima iende sanjari na mikakati ya Afrika kuhakikisha kwamba bara hilo na watu wake wanafaidika na matokeo yake wakiwemo wanawake na vijana. Sudan Kusini  kijana Vorna Joseph Zaki kutoka shirika la African Rising anaelezea umuhimu wa siku hii kwa vijana (SAUTI YA VERNO) "Tuna azimio la kilimanjaro  ambalo limepitishwa na vijana , tunataka kuwa na Afrika nchi na sio Afrika bara, tunaweza kwa kupanua wigo wa hatua za kisiasa na kiraia na tupiganie haki za wanawake na uhuru katika jamii zote, tudai utawala bora, tudai haki ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi, na tukitekeleza haya tutakuwa na bara bora" Akizungumzia umuhimu wa siku hii katika maendeleo, mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika ofisi ya Umoja wa Mataifa Balozi Modest Mero amesema. ( Sauti Mero)