Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa G7 chukueni hatua kulinda watoto- UNICEF

Viongozi wa G7 chukueni hatua kulinda watoto- UNICEF

Wakati viongozi wa kundi la nchi 7 zilizo na uchumi mkubwa zaidi wakijiandaa kukutana huko Italia, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limewasihi wapitishe mpango mkakati wenye vipengele sita vya kuhakikisha watoto wakimbizi na wahamiaji wanakuwa salama wanapovuka bahari ya Mediterania kusaka hifadhi Ulaya. Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Nats..

Dounia, mtoto mkimbizi mwenye umri wa miaka 11 sasa yuko Ugiriki, licha ya kwamba ana machungu mengi moyoni, ni nafuu kwake kwani si miongoni mwa watoto wapatao 200 waliofariki dunia mwaka huu pekee kwenye bahari ya mediterania wakivuka kutoka Afrika Kaskazini kwenda Ulaya kuokoa maisha yao.

Safari yao ilikuwa ya kuogofya kwani walikamatwa na kundi la Mafia..

(Sauti ya Dounia)

“Niliogopa sana kwa kuwa wangeweza kutuua na tumetoka mbali.. Afghanitan na sasa wametukamata, wanatishia kutuua, kuchukua fedha zetu na wasitufikishe hapa. Tunataka kuwa salama kama wakazi wa Ulaya. Kwa nini wao wana usalama sisi hatuna.”

UNICEF kupitia video kama hii inachagiza wadau wakiwemo viongozi hao wa G7 kupitisha vipengele hivyo ambayo ni pamoja na kulinda watoto wakimbizi na wahamiaji hususan wanaosafiri peke yao, kuachana na kuwaweka watoto hao korokoroni na kuhakikisha familia hazitenganishwi.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Justin Forsyth amesema kukutana kwa viongozi hao wa G7 huko Sicily mji hitimisho la safari ya matumaini na ya huzuni kwa watoto, ni fursa ya viongozi hao kuonyesha uongozi jasiri na kupitisha vipengele hivyo kwa maslahi ya watoto.