Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa UNESCO wapunguza ujinga Msumbiji

Mradi wa UNESCO wapunguza ujinga Msumbiji

Asilimia 57.8 ya wanawake na zaidi ya asilimia 30 ya wanaume katika mkoa wa Boane nchini Msumbiji hawajui kusoma wala kuandika, jambo ambalo linakwamisha watu hawa wazima katika uchangiaji wa maendeleo kwenye familia na jamii zao, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO hii leo.

Ili kukabiliana na idadi hiyo kubwa ya ujinga, mwaka 2015, shirika hilo lilivumbua mradi wa kuwafundisha na kuwawezesha watu wazima, wasichana na familia zao kusoma na kuandika hususan mashinani na kandokando mwa miji.

UNESCO inaendeleza mradi huo katika jamii 13 kutoka wilaya za Boane, Eráti na Memba inayotumia mbinu bunifu zenye kulenga ujumuishaji wa vizazi mbalimbali na jamii, na unaozingatia umuhimu wa mchango wa wazazi, wazee na walezi katika elimu ya mtoto.