Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado hali tete Sudan Kusini, nchi za ukanda zinusuru: Shearer

Bado hali tete Sudan Kusini, nchi za ukanda zinusuru: Shearer

Mwakilishi maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa umoja huo nchini humo UNMISS David Shearer, amesema bado machafuko yanaendelea nchini humo huku UNMISS ikiendelea kusaka suluhu ya mgogoro.

Akihutubia baraza la usalama kwa njia ya video kutoka mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, kiongozi huyo amesema kuendelea kwa machafuko hususani ya kikabila kunaongeza kudororoa kwa hali ya kibinadamu wakati ambapo utolewaji wa misaada unakwamishwa na mapigano.

Bwana Shearer amewaambia wanadiplomasia katika mkutano wa baraza la usalama wa kujadili hali nchini Sudan Kusini kuwa madhila kwa binadamu yanaongezeka mathalani kipindupindu ambapo visa zaidi ya 7000 vimeripotiwa.

Amesema nchi za ukanda huo hususani Afrika ya Mashariki zina ushawishi mkubwa katika kusaka suluhu ya kisiasa Sudan Kusini.

( Sauti Shearer)

‘‘Ninahamasisha nchi wanachama za ukanda huo kujihusisha na kusaka suluhu . Hata hivyo mshikamano na umoja wa ukanda ambao ni muhimu unatarajiwa.’’