Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamii nchini Sudan Kusini zakubaliana kuweka silaha chini

Jamii nchini Sudan Kusini zakubaliana kuweka silaha chini

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, David Shearer, leo ameshuhudia kusainiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, ikiwa ni pamoja na utekaji wa watoto na uporaji wa ng'ombe, kati ya makundi mawili hasimu ya Jonglei na Boma nchini humo.

Amesema mkataba huu ni hatua mojawapo kukiwa na mengine mengi yanayotakiwa kufanyika, kwani mfululizo wa mapigano makubwa kati ya vijana wa Dinka Bor na Murle yaliyosababisha vifo vya raia wengi, utekaji wa wanawake na watoto, vizuizi barabarani na uharibifu wa mali vinakiuka mkataba wa amani uliosainiwa Desemba 2016.

Ameongeza kuwa mkataba huu utatuliza hali ya hatari iliyokuwa inafuata hivi karibuni, ambapo maelfu ya vijana walijiandaa kupigana, na hivyo akatoa wito kwa serikali kuweka mfumo wa ufuatiliaji, kufuatilia utekelezaji wake na kuhakikisha unaheshimiwa.

Serikali ya Sudan Kusini imeishukuru UNMISS na jamii hizo katika kuwezesha mazungumzo ya amani, ikisema kuwa ukosefu wa usalama unaoendelea ni tatizo la taifa na hivyo ni lazima watumie fursa hiyo kujifunza kuishi pamoja kwa amani.