WHO yapata Mkurugenzi Mkuu mpya naye ni Ghebreyesus wa Ethiopia

23 Mei 2017

Dkt. Tedros Ghebreyesus wa Ethiopia, amechaguliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa shirika la afya duniani, WHO kwa kipindi cha miaka mitano .

Uchaguzi umefanyika hii leo kwenye makao makuu ya shirika hilo huko Geneva, Uswisi ambapo Ghebreyesus ameibuka mshindi baada ya kuwashinda wenzake wawili David Nabarro wa Uingereza na Sania Nishtar wa Pakistan.

Ghebreyesus ambaye anakuwa mwafrika wa kwanza kushika wadhifa huo, anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Dkt. Margaret Chan ambaye amemaliza muda wake baada ya kuhudumu kwa awamu mbili za kipindi cha miaka mitano mitano.

Mkuu huyo mpya wa shirika la afya ulimwenguni ambaye amewahi kushika nyadhifa mbali mbali za uwaziri nchini mwake ikiwemo Waziri wa Afya, ameahidi kufanikisha lengo la afya kwa wote akisema..

(Sauti ya Ghebreyesus)

"Kwa sasa, ni nusu tu ya wakazi wa dunia wana huduma ya afya bila kikwazo. Hii ni lazima iboreshwe haraka. mwelekeo uko bayana. Malengo ya maendeleo endelevu yanapatia WHO fursa ya kuongeza fursa za huduma ya afya kwa wote." 

image
Kutoka ukurasa wa Twitter wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, pongezi kwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa WHO.

Muda mfupi baada ya kutangazwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres amempongeza akisema ushindi wake utakuwa muhimu katika kuhakikisha maisha yenye afya na kukuza ustawi kwa wote  na kwa umri wote.Majina ya wagombea yalipitishwa tarehe 23 mwezi Septemba mwaka jana na nchi wanachama wa WHO ambapo baada ya hapo kulifanyika taratibu mbali mbali za mchujo hadi kubakia wagombea watatu waliopigiwa kura hii leo.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter